26/07/2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe, amefungua rasmi Warsha ya Uwasilishaji wa Matokeo ya Mchakato wa Kutafuta Destination Brand au Chapa ya Kiutalii ya Zanzibar, iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni Zanzibar.
Akifungua warsha hiyo, Dkt. Jumbe amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha ushindani wa sekta ya utalii katika soko la kimataifa kupitia mikakati ya kisasa ya utangazaji na ujenzi wa taswira imara ya Zanzibar k**a kivutio cha kipekee cha utalii duniani.
Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, kwa kushirikiana na Kampuni ya Technology Benchmark Ltd, wanaendelea na mchakato wa kuandaa Chapa ya Kiutalii ya Zanzibar itakayokuwa chachu ya kuitangaza Zanzibar katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi, kiutalii, kiutamaduni, kijamii pamoja na kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika soko la utalii duniani.
Dkt. Jumbe amesema chapa hiyo haitakuwa nembo au kaulimbiu pekee, bali itakuwa utambulisho rasmi wa Zanzibar utakaoonesha upekee wake, historia yake, urithi wa utamaduni, vivutio vya asili na fursa mbalimbali za uwekezaji na maendeleo ya uchumi, huku ikiweka msingi wa mkakati wa muda mrefu wa kuitangaza Zanzibar katika masoko ya kimataifa.
Aidha, amesisitiza kuwa mchakato huo umehusisha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na maendeleo ili kuhakikisha chapa itakayopatikana inaakisi utambulisho halisi wa Zanzibar na kuendana na dira ya Serikali ya kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii.
Kwa upande wake, wataalamu kutoka Kampuni ya Technology Benchmark Ltd waliwasilisha matokeo ya utafiti na hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kuandaa chapa hiyo, wakieleza kuwa mapendekezo yaliyowasilishwa yamelenga kuijenga Zanzibar k**a kitovu cha utalii wa kimataifa chenye utambulisho wa kipekee na wenye mvuto mkubwa kwa watalii na wawekezaji.
Mchakato huo umebeba kaulimbiu isemayo "Zanzibar, the Soul of the Indian Ocean" (Zanzibar, Roho ya Bahari ya Hindi), ambayo inalenga kuonesha upekee wa Zanzibar k**a kisiwa chenye urithi wa kihistoria, utamaduni , mazingira ya asili, na ukarimu.
Yawah Ben