17/10/2026
Leo, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mheshimiwa Mwanaidi Rajabu, ametembelea ofisi za UZIKWASA kukagua maandalizi ya kumpokea Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, anayetarajiwa kutembelea taasisi hiyo Jumatatu, tarehe 19 Oktoba 2026. Ziara ya Balozi inalenga kujionea shughuli zinazotekelezwa na UZIKWASA kwa ushirikiano na ufadhili wa Ubalozi wa Ireland wilayani Pangani.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mwanaidi Rajabu ametembelea Kituo cha Mafunzo cha UZIKWASA, ambacho kimerejeshwa baada ya kuharibiwa na moto mwezi Februari 2026. Tukio hilo lilisababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za taasisi kwa zaidi ya miezi saba. Ukarabati wa kituo hicho umerejesha nafasi muhimu ya kujifunza, kutafakari na kuchochea mabadiliko katika jamii. Pia ametembelea studio za Pangani FM, redio inayomilikiwa na UZIKWASA.
Awali, timu ya UZIKWASA, ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Novatus Urassa, ilikutana na Mkuu wa Wilaya ofisini kwake kumweleza kuhusu shughuli za taasisi na maandalizi ya ziara hiyo. Miongoni mwa shughuli zilizowasilishwa ni uanzishwaji wa Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto Shuleni, yatakayozinduliwa rasmi na Balozi Nicola Brennan wakati wa ziara yake.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amepongeza mchango wa UZIKWASA katika kuiwezesha jamii kushiriki katika maendeleo endelevu, hususan kupitia kushughulikia mila na desturi kandamizi zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.