ELIMU KITAA

ELIMU KITAA Kufundisha Namna Sahihi Ya Kulijua Kusudi La Mungu katika Maisha Yetu. Discovering Life's Purpose

KALAMU YANGU, RAI YANGU!HIVI, KAPTURA ZAKO ZOTE NI ZAKO KWELI NA ZINAKUENEA VIZURI MPENDWA!Wapendwa wasomaji wa makala z...
03/06/2025

KALAMU YANGU, RAI YANGU!

HIVI, KAPTURA ZAKO ZOTE NI ZAKO KWELI NA ZINAKUENEA VIZURI MPENDWA!

Wapendwa wasomaji wa makala zangu hamjambo? Mimi sijambo na niko tayari kwa safari yetu ya kutafakari kuhusu maisha. Mlinifurahisha kwa mrejesho wenu wa makala ya wiki jana ambayo ilimuuliza kila mmoja k**a ana salio kwenye bima yake ya kijamii. Endeleeni kusoma makala zangu ili niendelee kupata sababu za kuandika tena na tena.

Wiki hii ninaomba tutafakari kuhusu kaptura zetu. Kila mmoja ana kaptura yake. Hapa ninajua ushaanza kuwaza kaptura! K**a ni mwanamke ushaanza kujiweka pembeni ukijenga hoja kwamba kaptura ni za wanaume! Ni sawa, lakini kaptura ya makala yangu kila mmoja anayo na anaivaa. Unabisha! Funga mkanda tusafiri uone mwenyewe.

Kusema ukweli, uandishi ni raha. Tena, raha inakolea zaidi pale unapopata mrejesho wa wasomaji wako. Makala ya wiki iliyopita ilinipa raha zaidi kutokana na mawazo na unyumbufu wa tafakuri zenu. Mama yangu mmoja ambaye ni Profesa, aliniomba nimtumie makala ile ili asome. Nilipomtumia, mama huyo kwa kweli aliisoma kwa uaminifu. Alipomaliza, alinitumia mrejesho mzuri akisema makala inagusa mambo muhimu ya jamii zetu na akatamani kila mtu aisome. Zaidi, aliniombea nizidi kuandika tena na tena kwa ajili yako wewe unayesoma makala yangu na wengine. Alipomaliza kutoa mrejesho aliniuliza swali, "Lakini mwanangu, haya unayoyaandika huwa unayatoa wapi jamani? Baada ya kutafakari namna ya kumjibu mama, niliona niseme ukweli kwamba mengi ninayoyaandika ninayachota kwenye jamii zetu.

Jibu nililompatia Profesa, lilikuwa la kweli kabisa. Hata mada ya wiki hii nimeitoa kwenye jamii zetu kabisa. Nikiwa ninawaza wiki hii niandike kuhusu nini, nilijikuta ninaijiwa na mambo mengi kichwani. Katika matini zilizokuja kichwani, nilijikuta ninakumbuka mazungumzo kati ya daktari mmoja wa hospitalini na watu waliotaka kujua namna ya kumtibu mtoto mwenye shida ya kuweka kidole kinywani kila mara. Sijui unanielewa hapa!

Daktari alikuwa anaongea na watu ili kubadilishana nao mawazo. Alipoletewa kesi ya namna ya kumsaidia mtoto ambaye anasoma darasa la kwanza, anayetembea muda wote akiwa ameweka kidole cha mkono kinywani, alitoa ushauri ambao uliniacha hoi. Hapo ndipo nilipopata mada ya kuandikia makala ya wiki hii. Daktari alisema kwamba dawa ya mtoto mwenye tabia ya kuweka kidole mdomoni ni ndogo tu. Alisema kuwa mtoto huyo ukimshonea kaptura kubwa inayomzidi kiuno, utakuwa umemsaidia. Mtoto huyo akiwa anatembelea, badala ya kuweka kidole mdomoni, muda wote atatembea akiwa anashikilia kaptura yake na huenda baada ya wiki kadhaa tatizo la kuweka kidole mdomoni likaisha. Badala ya kuweka kidole kinywani, muda wote mtoto atakuwa anapambana na kaptura inayotishia kudondoka. Unaipata picha lakini! Kichwani unaona jinsi mtoto anavyoishikilia kaptura! Unaona anavyohangaika lakini na kusahau kulamba kidole chake?

Nikiwa ninacheka baada ya kukumbuka stori ya Daktari kuhusu matibabu ya mtoto kwa kumshonea li-kaptura li-kubwa, nilijikuta akili inahamia huko Namagondo - Ukerewe, Mwanza nyumbani kwa Prof. E. Kezilahabi. Kwa kweli, nimelazimika kumkumbuka nguli na jabali la fasihi, Prof. Euphrase Kezilahabi ambaye sasa ni marehemu (Hayati!!). Huyu mwamba aliandika sana kazi za kifasihi ambazo zinafikirisha sana.

Tafakuri yangu imezama katika tamthilia yake moja inayoitwa Kaptura la Marx. Nilipohusianisha kisa cha kaptura kubwa ya dogo anayeweka kidole mdomoni na visa vya Kaptura la Marx nilijikuta ninaangua kicheko. Ni kicheko ambacho kinatangulia tafakuri. Kwa hakika, baada ya kicheko, kinachofuatia ni huzuni. Ni huzuni ndiyo!

Katika tamthilia hiyo, Prof. Kezilahabi anaonesha kwamba baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika, baadhi ya viongozi wa bara hili walikopa na kuiga itikadi na mifumo ya kigeni bila kuielewa vizuri namna ya kuitekeleza. Viongozi hao walijikuta wanasafiri weee bila kufanikiwa na hatimaye kuwasababishia maisha magumu wananchi wao. Wanasema, asiyejua anakoelekea, hapotei. Kinyume chake, ukiona mtu anasema kwamba amepotea njia, maana yake anajua alikuwa anaelekea wapi. Hali hii ni tofauti na watawala wanaozungumziwa katika tamthilia hii. Watawala hawa, wala hata hawajui k**a wamepotea bali huendelea husukumiza mbele wananchi na kuwaswaga k**a mbuzi ili waende nao. Shida kubwa, kwa mujibu wa tamthilia hii, ni watawala wa Kiafrika kutokaa chini na kutafakari kwa kina, ni itikadi na mifumo ipi ambayo ni mwafaka kwa Waafrika katika mazingira yao wenyewe. Huku ndio kucheza ngoja ya jirani kikasuku au kuvaa kaptura za watu hata k**a hazituenei. Kwa kuwa siasa si uwanja wangu, ngoja niishie hapo kuhusu tamthilia ya Kaptura la Marx.

Pamoja na kwamba nimeachana na mambo ya watawala, basi mimi na wewe tujikague k**a nasi tumevaa kaptura ambazo ni zetu na zinatuenea. Ngoja nianze kwa kukugeukia kidogo: Swali la kwanza, hiyo kaptura yako uliyovaa una uhakika ni yako kweli? Swali la pili, kaptura hiyo inakuenea? Twende na maswali hayo na ninakuhakikishia kwamba kwa wiki hii walau yanatutosha.

Katika kutafakari namna tunavyoishi, nimekumbuka stori za kijiweni. Ninasema ni za kijiweni kwa sababu sina uhakika sana k**a ni za kweli. Nikiwa kijiweni nilikutana na stori ambazo wewe na mimi tunaweza kuzitafakari na kuona k**a zina ukweli au la.

Katika stori ya kwanza, jamaa mmoja alipomaliza chuo, alipata ajira serikalini. Kwa mwezi, jamaa alikuwa analipwa S*T. 1,200,000/= baada ya makato yote. Kabla ya ajira, jamaa alikuwa na ndoto ya kununua gari zuri aina ya BMW katika maisha yake. Alisononeka sana alipokuwa anaona watu mitaani wanamtimulia vumbi na magari hayo mazuri. Akasema, siku Mungu akimjalia, ipo siku naye atawakomesha. Mara tu alipoajiriwa na kugundua kwamba kuna fursa ya kukopa kwa miaka 9, haraka alienda kukopa benki na akanunua BMW yake fasta. Gari lile lilimtesa sana kwani alishindwa kumudu gharama za mafuta na matengenezo yake. Maisha yake yakawa magumu sana kwa sababu, mkopo ule ulimfanya hata kula yake iwe duni. Alianza kuwaza kwamba huenda kuna mtu kamroga asiendelee k**a wengine mitaani. Huyu unadhani kaptura aliyokimbilia kuvaa ilikuwa yake! Je, ilimwenea! Angalia jinsi alivyoishia kutembea kila siku akiishikilia isidondoke. Huyu, k**a yule dogo tu bwana! Usicheze na kaptura za watu aisee!

Katika stori ya pili, kuna jamaa mwingine alipomaliza masomo ya chuo kikuu na kuona ajira hazieleweki, aliamua kufanya tathmini ya kibiashara katika eneo analoishi. Alibaini kwamba eneo lile lilihitaji huduma ya duka la mazao. Hivyo, aliomba mtaji kidogo kwa ndugu na akafungua duka. Alikuwa ananunua mazao mikoani na kuweka dukani kwake. Alianza kidogo na taratibu akakua, duka likawa kubwa sana. Wateja walizoea duka lile na jamaa akawa ametoka kimaisha.

Baada ya muda mrefu kidogo, kijana mwenzake aliyemaliza naye chuo alimtembelea na kuona hatua aliyopiga. Alimuonea wivu sana rafiki yake kwa mafanikio yale. Katika kuongea na watu wa pale, kijana akaambiwa kwamba kuna fremu ya biashara jirani na pale, inapangishwa. Naye, kwa haraka akatafuta kitu cha kuweka dhamana, akakopa fedha benki. Alifungua duka la nafaka pembeni ili amnyang'anye wateja rafiki yake. Kitu cha kushangaza, duka lake halikuchanganya. Lilikuwa halikui kwa sababu ya kukosa wateja. Mwishowe, alifunga duka na kumchukia rafiki yake na akaanza kusema kwamba rafiki yake ni mshirikina na mfuasi wa Freemasons. Unadhani huyu alikosea wapi? Kaptura aliyokimbilia kushona ilikuwa yake?

Mpendwa msomaji wangu, mimi na wewe nasi tuna kaptura zetu. Hizi ni zetu kweli na zinatuenea? Katika safari ya tafakuri hii, wala usipotee njia. Ninachokuambia tu ni kwamba kabla ya kufanya au kutekeleza mikakati yetu, tufanye utafiti, tufanye tathmini kisha tuvae hizo kaptura zetu. Tusipofanya hivyo, maendeleo tutaendelea kuyasikia kwa watu. Kila mara tutakuwa tukipambana na kaptura zetu zisizotuenea ambazo mara zote zinataka kudondoka. Kwa sababu ya kuvamia kaptura za watu ndiyo maana tuna wanamuziki wasiovutia, waandishi wa vitabu visivyo na mvuto, walimu wa ovyo, madereva wa ovyo, wanasiasa wachumiatumbo, kwa kutaja wachache tu. Sasa na wewe usiniulize kuhusu kaptura yako. Itafute kisha pima k**a inakuenea au la! Kila la heri.

Tukutane tena Jumatatu ijayo. Asante sana kwa kusoma makala yangu.

=============

©️ Leonard Bakize, 2025
Mwalimu wa uandishi, mwandishi, mhariri, mfasiri na mchapishaji
26.05.2025
+255 755 643 590
[email protected]

********

Natamani kuwa 'chawa',Nisifie matajiri,Kazi ya kuajiriwa,Yanitia ufakiri.Niwaseme kwa mazuri,Wovu nipake sukari,Nami nii...
03/06/2025

Natamani kuwa 'chawa',
Nisifie matajiri,
Kazi ya kuajiriwa,
Yanitia ufakiri.

Niwaseme kwa mazuri,
Wovu nipake sukari,
Nami niishi vizuri,
Maisha ya kifahari.

Natamani kuwa 'chawa',
Nimsifie mbunge,
Japo hakuchaguliwa,
Acha nimpangepange.

Nipongeze zake hoja,
Yani nimvike koja,
Nidanganye ana tija,
Nitimize zangu haja.

Natamani kuwa 'chawa',
Nimpetipeti bosi,
Wenzangu wasivyopewa,
Nivipate kirahisi.

Nimpempe umbea,
Watu wanayoongea,
Yote na yeye kushea
Michongo kujizolea.

Natamani kuwa 'chawa',
Nimsifie Rais,
Binti yangu kuolewa,
Yeye katoa nafas.

Nisichoke msifia,
Nijisafishie njia,
Hwenda atafurahia,
Cheo atanipatia.

Mohamedi A. Ngunguti
(Jingaerevu) - DSM, Tz

KALAMU YANGU, RAI YANGU!SEMA UKWELI RAFIKI, UMESHADANDIA MAGARI MANGAPI MPAKA SASA!Mpendwa msomaji wangu, karibu tena ka...
03/06/2025

KALAMU YANGU, RAI YANGU!

SEMA UKWELI RAFIKI, UMESHADANDIA MAGARI MANGAPI MPAKA SASA!

Mpendwa msomaji wangu, karibu tena katika ulingo wa kutafakari kuhusu maisha yetu ya kila siku. Ninaendelea kukushukuru kwa kusoma. Ni kwa sababu yako, mimi ninaendelea kuandika sasa.

Wiki hii ninaomba kalamu yangu ikutafakarishe kuhusu magari ambayo umeshadandia na kushuka. Ili twende sawa, hebu vuta kumbukumbu na ujiulize ushadandia magari mangapi na ukashuka! Ushawahi kuona gari zuri kwa mbali na likifika karibu na wewe unarukia, kisha unashuka baada ya kushindwa kustahimili mikiki ya gari hilo!

Mimi nimeshadandia mengi mpaka sasa. Na wewe ukiwa mkweli, lazima utanipatia ushuhuda. Ngoja nianze mimi kisha nawe ukishasoma, nipe ushuhuda wako.

Kusema ukweli kabisa, mpaka sasa nina makovu mengi ya kudandia magari na kushuka. Kuna wakati huwa ninajiuliza sasa gari langu hasa ni lipi? Haya magari niliyonayo sasa yananifaa na ninayaendesha vizuri kweli au ninayaburuza tu ovyo ilimradi safari iwe safari?

Mimi nilianza kudandia magari nikiwa kijana mdogo kabisa. Wakati fulani, nilipoona Wachina kwenye video wakicheza Karatee, Kung-Fu na Taikwondo, nilivutiwa sana na nikawa mtazamaji na mfuatiliaji mzuri wa michezo hiyo. Matokeo yake, nilipopata fursa nikiwa ninasoma kidato cha 1-4, nilijiunga na kikundi cha mazoezi milimani na huko nikasoteshwa kwenye mawe na kokoto eti nikomae. Jamaa yetu ambaye mpaka sasa tunamwita Vandame alitusotesha kwelikweli aisee! Ingawa ni rafiki yangu, lakini nikikumbuka hili, huwa ninacheka sana. Jamaa kwenye hili hakuwa na huruma. Baada ya kuona hali ni tete, nilipopata upenyo, nilitoroka haraka. Bahati nzuri, ukitoroka, Vandame wetu alikuwa hakufuatilii tena. Mpaka leo nimeamua kuwa mpenzi mtazamaji wa Kareti, Kung-Fu na mengineyo. Sitaki kabisa kufanya hayo. Kwa sasa nikiingia huko, na jinsi nilivyokomaa, watanivunja bure! Hilo gari acha tu liende bwana! Mliomo humo endeleeni na safari.

Wakati fulani, nilianza kufuatilia mchezo wa mpira nikiwa mdogo na nikawa ninapenda sana jinsi watu wanavyoshangiliwa na kufunga magoli. Nami nilianza kucheza "vibhangebhange" (mipira ya kutengeneza kutokana na nguo chakavu) ili niwe mchezaji. Tukiwa tunacheza na watoto wenzangu, siku moja jamaa alinitwanga mpira wa tumbo. Nilihisi kufa. Nilipotoka hapo, niliviacha vya mpira siku hiyohiyo na mpaka leo sijarudia na wala sina mpango kabisa. Lakini kukiwa na mechi aaaa lazima nitazame. Kuingia uwanjani, hapana kwa kweli! Lile shuti la tumbo mpaka leo sijalisahau. Hilo gari, acha tu liende.

Nikiwa katika masomo ya shule ya msingi, wakati huo kulikuwa na mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira, riadha, kuruka juu na chini, kurusha kitufe, n.k. Kulikuwa na wanafunzi wazuri sana wa riadha. Nilikuwa ninavutiwa sana na jinsi wakimbiaji walivyosifiwa wakikimbia na kushinda. Siku moja na mimi nikajiambia, "Kwani nikifanya mazoezi si na mimi ninaweza kushinda k**a hao!" Basi siku moja wakati wa pumziko, rafiki zangu walikuwa wanaelekea uwanjani na mimi nikaamua kuwafuata ili nifanye mazoezi. Wakiwa wanabishana kwamba nani anaweza kumshinda mwenzake, na mimi niliamua kuungana nao ili nijipime. Tulipanga mstari na kupewa ishara ya kuanza mbio. Tulitoka spidi kwelikweli! Hata kabla hatujafika katikati ya mbio, nilijikuta nikiwa wa mwisho. Nilipowatazama wenzangu, hao wako mbali! Nilipojaribu kuongeza mwendo, nilibanwa na kichomi hicho aisee, nikasema cha kufia nini! Niliamua kukaa chini nipumzike. Kuanzia hapo, sijakimbia tena kimashindano mpaka leo. Lakini nikiamua kukimbiza kuku, mbuzi au kondoo, ninamk**ata vizuri tu. Nimeshakubali kwamba mimi ni mtazamaji wa mbio. Wenye mbio zao wakimbie bwana! Hilo gari nalo, acha liende tu.

Tukiwa watoto, kulikuwa na mtoto mwenzetu ambaye alikuwa mtaalamu wa sarakasi. Hata sijui alikuwa amejifunzia wapi bwana! Alikuwa anapiga kinyume mpaka tunampatia zawadi za makofi. Tukipata vitumbua kutoka kwa wazazi tulikuwa tunampelekea ili atupigie kinyume. Siku moja nikiwa mwenyewe nami nikasema kwani nikipiga kinyume nikaweza, na mimi si watakuwa wananipa vitumbua! Ndugu yangu, nilikwenda kwenye makapi ya maharage ili nisiumie. Nilipojaribu kubinuka kinyume, niliangukia kichwa. Nilipotoka hapo, shingo iliniuma sana. Kuanzia siku hiyo, mpaka leo sijawahi kujaribu tena kupiga kinyume. Ila nikiona wengine wanafanya, roho inauma sana maana bado ninatamani. Hata hivyo, hilo gari nalo acha tu liende.

Zaidi ya hayo, niliwahi kuwa fundi wa redio wa kijiji huko kwetu Biturana, Kibondo- Kigoma. Enzi hizo, ninakuambia, niliwika kwelikweli. Nilifahamika kwa watu wa rika zote wenye redio zao. Wazee wenye redio za Mkulima, Panasonic, Artech, Philips, n.k walikuwa wananipenda kwa sababu wakileta redio nilikuwa ninazinyoosha kwelikweli. Kupitia kazi hiyo, nilifanikiwa kuwasaidia wazazi katika mahitaji mbalimbali ya shule kwa sababu wakati huo nilikuwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Malagarasi-Kibondo. Kupitia kazi ya ufundi, nilijikuta ninapenda muziki. Kutokana na usuli huo, baadaye nikiwa kidato cha tano na sita huko Babati - Manyara si nikajiunga na kwaya! Mwalimu alifundisha weee lakini wapi! Mara ooo mdomo uwe na oval shape, mara tule mayai sauti ziwe nzuri lakini mimi wapi! Tukienda kuimba nilikuwa ninajificha katikati ili nisiwaharibie wenzangu wanaojua. Baada ya kumaliza kidato cha sita na masomo ya chuo kikuu na kuanza maisha, nilipofuatilia sana wapiga kinanda, nilivutiwa mno mpaka na mimi nikakinunua ili nijifunze. Baadaye nikiwa nchini Zimbabwe nilipata mwalimu na nikamwomba awe ananifundisha nyumbani. Mwalimu alikuwa mzuri kwelikweli, lakini mimi kuelewa waapi! Akinifundisha mambo ya nota, nilikuwa nayaona k**a madudu tu. Hatimaye, nilikubaliana na mke wangu tukigawe kinanda ili kisiharibike. Lakini mpaka sasa napenda kutazama na kusikiliza nyimbo za kwaya. Sasa ukiniambia niwe mwanakwaya, hapana kwa kweli. Hilo gari acha liende.

Katika matukio mbalimbali ya sherehe za harusi, huwa ninavutiwa sana na mchezo wa Kwaito. Nikiona watu wanacheza Kwaito, wakati mwingine ninajikuta nishanyanyuka na kwenda kuungana nao. Lakini kwa kuwa ninajua sijui kucheza kwa stepu stahiki, basi huwa ninajificha katikati ya watu ili nisiwaharibie kumbukumbu za picha na video wenye harusi zao. Nimeshajaribu sana, lakini gari la Kwaito mhuuu, limenishinda kabisa mpaka leo.

Mpendwa msomaji wangu, katika maisha yetu tunakutana na mengi. Kupitia kujaribu na kishindwa, hatimaye tunapata yanayoendana nasi. Makala yangu haina lengo la kukukatisha tamaa katika kujaribu vitu katika maisha. Ninasisitiza tu kwamba unapoona watu wamefanikiwa leo, ujue kwamba huenda walijaribu na kushindwa katika mambo mengi mpaka wakapata yale yanayoendana nao leo. Hata nawe unapoona k**a vile hakuna uelekeo, basi usiogope.

Ni lengo langu kukutia moyo kwamba nawe yapo yanayokufaa na ambayo unayamudu vizuri. Katika maisha yetu, lazima tukubali kwamba kuna magari ambayo hayaendani nasi kwa sababu mbalimbali. Kuna wakati lazima ukubali tu kuwa mpenzi mtazamaji wa magari na si dereva wala abiria. Ukitaka kupanda kila gari, utapata tabu sana.

Katika kutafakari ujumbe wa makala yangu, jiulize k**a mpaka sasa ushapata gari linalokufaa au bado unadandia na kushuka. K**a hujapata, basi kuwa makini na usichoke kuchunguza mpaka upate gari lako. K**a unajilazimisha kusafiria gari ambalo haliendani na wewe, basi utafika ukiwa umechoka sana na huenda usifike unakoelekea. Kaa chini, chekecha mpaka upate gari lako. Baada ya hapo, endelea na safari yako. Ninakutakia safari njema.

Asante sana kwa kutenga muda wako na kusoma makala yangu. Tukutane tena Jumatatu ijayo.
______

©️ Leonard Bakize, 2025
Mwalimu wa uandishi, mwandishi wa vitabu na makala, mhariri, mfasiri na mchapishaji
+255 755 643 590
02 Juni 2025
[email protected]
===============

Wape Wengine Kazi kwa Ajili Yako: Tumia Juhudi Zao Kufikia Malengo YakoKatika ulimwengu wa biashara na mahusiano ya kija...
23/05/2025

Wape Wengine Kazi kwa Ajili Yako: Tumia Juhudi Zao Kufikia Malengo Yako

Katika ulimwengu wa biashara na mahusiano ya kijamii, uwezo wa kushirikiana na wengine ni muhimu sana. Sheria ya "Wape Wengine Kazi kwa Ajili Yako" inatoa mwanga juu ya jinsi ya kutumia juhudi za watu wengine ili kufikia malengo yako, bila ya kuwa na mzigo wa kazi zote mwenyewe. Hapa kuna maelezo ya kina kuhusu sheria hii na jinsi inavyoweza kutumika kwa ufanisi.

Maana ya Sheria
Sheria hii inasisitiza umuhimu wa kujenga mtandao wa nguvu wa watu wanaoweza kusaidia katika kutimiza malengo yako. Badala ya kufanya kila kitu peke yako, unapaswa kutafuta watu ambao wana ujuzi, rasilimali, au maarifa ambayo yanaweza kuongeza thamani kwenye mipango yako.

Faida za Kutumia Wengine
Kuokoa Wakati na Nguvu: Kwa kutoa kazi kwa wengine, unaweza kujielekeza kwenye majukumu muhimu zaidi ambayo yanahitaji ujuzi wako wa kipekee.

Kujenga Mahusiano: Ushirikiano unakuza uhusiano mzuri na watu. Hii inaweza kuleta fursa zaidi katika siku zijazo.

Upatikanaji wa Ujuzi Mbalimbali: Watu tofauti wana ujuzi tofauti. Kwa kushirikiana nao, unaweza kupata mtazamo mpya na mbinu bora.

Kujifunza na Kukua: Kazi na wengine inakupa nafasi ya kujifunza kutoka kwao, kuboresha ujuzi wako, na kuboresha uwezo wa kuongoza.

Jinsi ya Kutumia Sheria Hii
Tafuta Watu Wanaofaa: Kila mtu ana nguvu zake. Tafuta wale ambao wana ujuzi au ujuzi ambao unahitajika kwa mradi wako.

Wape Mwelekeo Dhahiri: Wakati unawapa watu kazi, ni muhimu kutoa maelekezo ya wazi na malengo ya wazi. Hii inasaidia kuondoa mkanganyiko na kuhakikisha kwamba kila mtu anafahamu jukumu lake.

Tafuta Ushirikiano wa Wakati: Usijifungie kwenye ushirikiano wa muda mrefu tu. Wakati mwingine, ushirikiano wa muda mfupi unaweza kuleta matokeo bora.

Kutoa Mshik**ano: Mtu unayemshirikisha anapaswa kuhisi kwamba kazi yao inathaminiwa. Toa mrejesho mzuri na uonyeshe shukrani kwa juhudi zao.

Jifunze Kutoka kwa Wengine: Pata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wale unawapa kazi. Hii itakusaidia kuboresha mbinu zako na kuongeza ufanisi wako.

Hitimisho
"Wape Wengine Kazi kwa Ajili Yako" ni sheria yenye nguvu ambayo inaweza kubadilisha jinsi unavyofanya kazi na kufikia malengo yako. Kwa kutumia juhudi za wengine, unaweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kufanikiwa, huku ukijenga mtandao wa ushirikiano na mahusiano mazuri. Kumbuka, nguvu ya pamoja ina uwezo wa kuzalisha matokeo makubwa zaidi kuliko juhudi za mtu mmoja pekee.

Address

Kididimo
Morogoro

Opening Hours

Monday 06:00 - 22:00
Tuesday 06:00 - 22:00
Wednesday 06:00 - 22:00
Thursday 06:00 - 22:00
Friday 08:00 - 22:00
Saturday 08:00 - 22:00

Telephone

+255764257495

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when ELIMU KITAA posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to ELIMU KITAA:

Share