03/02/2026
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO: 1 WAFALME 1:1-53 JUMATATU 02/02/2025
1 Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto.
2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto.
3 Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.
4 Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.
5 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake.
6 Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.
7 Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata.
8 Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia.
9 Adonia akachinja kondoo, na ng'ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme;
10 ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao.
11 Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari?
12 Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani.
13 Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia?
14 Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako.
15 Basi Bath-sheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme.
16 Bath-sheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini?
17 Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa Bwana, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi.
18 Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari.
19 Tena amechinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita.
20 Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu.
21 Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu.
22 Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia.
23 Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi.
24 Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi?
25 Maana leo ameshuka, na kuchinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia!
26 Walakini mimi, mimi mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi.
27 Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?
28 Ndipo mfalme Daudi akajibu, akasema, Niitieni Bath-sheba. Basi akaingia ndani kwa mfalme, akasimama mbele ya mfalme.
29 Naye mfalme akaapa, akasema, Bwana aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote,
30 hakika yake nitafanya leo k**a vile nilivyokuapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu.
31 Ndipo Bath-sheba akainama kifudifudi, akamsujudia mfalme, akasema, Bwana wangu mfalme Daudi na aishi milele.
32 Naye mfalme Daudi akasema, Niitie Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada. Nao wakaingia ndani mbele ya mfalme.
33 Naye mfalme akawaambia, Twaeni pamoja nanyi watumishi wa bwana wenu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu wangu mimi mkamtelemshe mpaka Gihoni;
34 kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na wamtie mafuta huko, awe mfalme juu ya Israeli; kapigeni panda, mkaseme, Mfalme Sulemani na aishi!
35 Kisha pandeni juu nyuma yake, naye atakuja ili aketi katika kiti changu cha enzi; kwa maana atakuwa mfalme badala yangu; ndiye niliyemweka awamiliki Israeli na Yuda.
36 Basi Benaya, mwana wa Yehoyada, akamjibu mfalme, akasema, Amina; Bwana, Mungu na bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo.
37 K**a vile Bwana alivyokuwa pamoja na bwana wangu mfalme, kadhalika na awe pamoja na Sulemani, na kufanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.
38 Basi wakashuka Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa mfalme Daudi, wakampeleka mpaka Gihoni.
39 Na Sadoki, kuhani, akatwaa ile pembe ya mafuta katika Hema, akamtia Sulemani mafuta. Nao wakapiga panda; na watu wote wakasema, Mfalme Sulemani na aishi!
40 Kisha watu wote wakapanda juu nyuma yake, watu wakapiga mazomari, wakafurahi furaha kubwa mno, hata nchi ikapasuka kwa sauti zao.
41 Basi Adonia, na wageni wote waliokuwa pamoja naye, wakasikia hayo walipokuwa wamekwisha kula. Naye Yoabu aliposikia sauti ya panda alisema, Za nini kelele hizi za mji uliotaharuki?
42 Naye alipokuwa katika kunena, tazama Yonathani, mwana wa Abiathari kuhani, akafika. Naye Adonia akasema, Karibu; maana wewe u mtu mwema, unaleta habari njema.
43 Naye Yonathani akajibu, akamwambia Adonia, Hakika bwana wetu mfalme Daudi amemtawaza Sulemani.
44 Tena mfalme alipeleka pamoja naye Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Wakerethi, na Wapelethi, wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme.
45 Kisha Sadoki, kuhani, na Nathani, nabii, wakamtia mafuta huko Gihoni, ili awe mfalme. Nao wamepanda juu kutoka huko wakifurahi, hata mji ukavuma. Ndizo kelele zile mlizozisikia.
46 Na tena, Sulemani ameketi katika kiti cha enzi cha ufalme.
47 Na tena, watumishi wa mfalme walifika, ili wambariki bwana wetu mfalme Daudi, wakisema, Mungu wako na alikuze jina la Sulemani kuliko jina lako, na kukifanya kiti chake cha enzi kuwa kitukufu kuliko kiti chako. Naye mfalme akainama chini juu ya kitanda chake.
48 Na tena, mfalme akasema hivi, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenipa leo hivi mtu wa kuketi katika kiti changu cha enzi, nayo macho yangu yakiwa yanaona hayo.
49 Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake.
50 Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu.
51 Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga.
52 Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.
53 Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.
🍞 MKATE WA LEO NA WACHUNGAJI:
|| 1 Wafalme 1:1–53. Ufalme Waahidiwa kwa Sulemani.
❓ Swali la Mwanzo: Je, unautafuta uongozi wa Mungu unapokabili hila na tamaa za madaraka duniani?
🪔 UTANGULIZI NA MUKTADHA
Sura hii inaanza na mfalme Daudi akiwa mzee na dhaifu. Anahitaji msaada wa kijana Abishagi kumtunza na kumfurahisha. Mwanawe Adoniya anajitangaza kuwa mfalme na kuandaa sherehe ili kujihakikishia wafuasi. Lakini nabii Nathani na Bathsheba wanamkumbusha Daudi ahadi kwamba Sulemani ndiye atakayerithi kiti cha enzi. Daudi anafanya mpango wa kumtawaza Sulemani hadharani, na Adoniya anabaki bila uungwaji mkono. Mwandishi wa 1 Wafalme anaelewa saikolojia yetu; wakati wa mafanikio, watu wanaweza kuanza kuona nafasi za madaraka k**a haki yao badala ya zawadi ya Mungu. Hili linaonekana katika kujitangaza kwa Adoniya na hofu yake ya kupoteza mamlaka.
📖 Soma Kwanza
Soma 1 Wafalme 1 na uangalie jinsi rushwa ya mwanadamu na mapenzi ya Mungu
📚 MUUNDO WA MADA KWA SURA HII
🪢1. Mzee Daudi na Abishagi (mst. 1–4): Daudi ni mzee na hawezi kuipasha mwili joto, hivyo wanamletea Abishagi kumtunza.
🪢2. Adoniya ajitangaza mfalme (mst. 5–10): Adoniya anajikusanyia magari na jeshi; anajiita mfalme na anafanya karamu bila kumwalika Nathani au Sulemani.
🪢3. Nathani na Bathsheba wanamkumbusha Daudi (mst. 11–27): Nathani anamwambia Bathsheba amkumbushe Daudi ahadi yake na kumwonya dhidi ya njama ya Adoniya.
🪢4. Sulemani anatawazwa (mst. 28–40): Daudi anamwita Sadoki, Nathani na Benaya; wanamtawaza Sulemani kwa mafuta na kumweka juu ya nyumbu wa mfalme na mji wote unashangilia.
🪢5. Adoniya anaogopa (mst. 41–53): Adoniya anasikia kelele za taifa; anapokimbilia madhabahuni, Sulemani anamwachia kwa sharti la kuwa uaminifu kwake.
🪔 MUHTASARI WA MADA
🌴1. Kisa kinaonyesha jinsi ahadi za Mungu zinavyoshinda mipango ya mwanadamu.
🌴2. Hata k**a Adoniya alikuwa mwana mkubwa wa Daudi aliye hai, Mungu alimteua Sulemani.
🌴3. Nathani na Bathsheba wanacheza nafasi ya muhimu ya kutetea ahadi za Mungu.
🌴4. Mwandishi anaonyesha hali ya saikolojia: usalama wetu wa kweli uko katika uaminifu kwa ahadi za Mungu, si katika hila.
🌴5. Yesu atasimamia utimizwaji wa ahadi ya Mungu ya kutufanya warithi wa kiti cha ufalme wa Mungu aliotuahidi.
👥 MASWALI YA KUJADILI: 1 WAFALME 1:1-53
✅1. Je Daudi aliyekuwa na wake wengi alikuwa na ulazima wa kutafutiwa binti mwingine mdogo wa kumtia joto? Je mara nyingi uzee huja na hali ya kujihisi upweke na maamuzi ya kutatanisha? Kipi bora kati ya wazee kuwekwa kwenye kambi za kuwatunzia au kuishi nao majumbani mwetu? Je ni lazima kila uzee uwe na changamoto k**a alizopitia Daudi? Unadhani kuna ukomo wa mtu kutumika kwenye nafasi za utumishi wa watu ili kuepuka mambo ya aibu yatokanayo na uzee?
✅2. Kitendo cha Abigaili kumpigania mwanae wa kiume asikose kiti cha kifalme unakifananishaje na kitendo cha Rebeka kumpigania Yakobo kuwa mrithi wa Isaka? Je wanaume wanazeeka mapema kuliko wake zao? Wasaidizi wa mfalme wa Daudi mara nyingi walikuwa washauri na walezi wa familia ya mfalme. Unaiona hali hiyo kwa wasaidizi wa viongozi wa kiroho wa leo? Unadhani familia ya kiongozi wa kiroho inahitaji mlezi?
✅3. Sisi tuliomwamini Yesu tumeahidiwa urithi wa kiti cha enzi na ufalme (Ufunuo 3:21: Luka 12:32). Unadhani kuna uwezekano wa ahadi hiyo iliyotolewa kwa viapo kutotimia kwetu badala yake kuelekezwa kwa viumbe wengine? Je viumbe wengine watalipokeaje wazo hilo la kutufanya sisi tulioanguka dhambini kuwa warithi wake? Je umemuandaa atakayekurithi?Je ni kweli kuwa urithi ambao watoto wako hawataugombania ni elimu na ujuzi unaowapa? Vipi ikiwa mtoto mwingine hazingatii hata hiyo elimu unayompa?
✅4. Je ni nini kilichomsukuma Adonia kuutambua ufalme wa Sulemani wakati ambao alikuwa ametawazwa? Je ni rahisi kumtii kwa dhati mtu uliyevumisha kwa watu kuwa hawezi uongozi? Je Sulemani alifanya sahohi kutomwadhibu Adonia kwa uasi wake? Katika maisha yako, ni njia zipi watu hutumia kupata madaraka bila kushirikisha mapenzi ya Mungu?Je, umewahi kuchezwa katika mpango wa mtu mwingine kwa sababu hawakutaka kutii mapenzi ya Mungu? Ungejifunza nini kutoka Nathani na Bathsheba?
🔍 MASWALI YA TAFAKARI
🍞1. Je, kuna eneo ambalo unaona umefanya mipango bila kumuuliza Mungu? Unashirikianaje na wale wanaokukumbusha ahadi za Mungu badala ya wale wanaotaka tu kukupandisha kwenye hadhi usiyostahili?
🧱 MATUMIZI MAISHANI
Andika ahadi za Mungu kuhusu wito wako na uzihifadhi mahali pa wazi. Omba hekima ya kushirikiana na watu k**a Nathani wanaokusaidia kukukumbusha ahadi hizo.
NENO LA KUTIA MOYO
Naye mfalme akaapa, akasema, Bwana aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zote, hakika yake nitafanya leo k**a vile nilivyokuapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, nikasema, Kwa yakini Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, naye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi badala yangu. (1 Wafalme 1:29-30).
NENO LA BARAKA
Kelele za wapinzani zisikuchanganye—utiwe nguvu kusubiri wakati wa Mungu, kwa maana baraka yako itathibitishwa hadharani. Amani ya Bwana ikaenee juu ya nyumba yako, na ufalme wa haki, amani, na furaha ukae moyoni mwako. Upendo, heshima, na umoja vikaimarishwe katika familia yenu kila siku. Nyumba yenu iwe mahali pa uwepo wa Mungu, pa faraja, uponyaji, na mwanzo mpya. Amina.
TAMKO LA IMANI
Ninatamka kwa imani kwamba mipango ya Mungu juu ya maisha yangu haitabatilishwa. Hata k**a sauti nyingine zitainuka kabla ya wakati, mapenzi ya Bwana pekee ndiyo yatakayosimama. Natamka kwamba kile Mungu alichoahidi kitatimia kwa wakati wake kamili. Sitachanganyikiwa na kelele za nje, wala kuogopa ushindani usiotokana na Mungu. Ninasimama katika amani, nikijua Mungu anatawala.
🔑 SALA YA MWISHO
Mungu mwenye haki, nakushukuru kwa ahadi zako zisizobadilika. Nisaidie kuzikumbuka na kutafuta mapenzi yako zaidi ya kutafuta madaraka. Niwezeshe kuwa mwaaminifu na mwenye busara k**a Nathani na Bathsheba, nikitetea ahadi zako dhidi ya njama na hila za kibinadamu. Amina.
👤 Watayarishaji wa Mwongozo huu wa Biblia: Pr. Stephen Letta, na Pr. Enos Mwakalindile, Dar es Salaam, 🇹🇿.