21/01/2026
Taasisi ya imeshiriki katika hafla ya utoaji wa hundi za mfano za mikopo ya asilimia kumi (10%) kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Mhe. Hamoud Abuu Jumaa, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa mikopo hiyo, akibainisha kuwa ni chachu muhimu ya kuinua uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya Halmashauri. Aidha, amewataka wataalamu wa halmashauri kusimamia kwa karibu matumizi ya mikopo hiyo ili ihakikishe inaleta tija iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bi. Shukuru Lusanjala, amesema jumla ya vikundi 54 vitanufaika katika awamu ya kwanza ya mikopo hiyo. Kati ya vikundi hivyo, 34 ni vya wanawake, 13 vya vijana na 7 vya watu wenye ulemavu, hali itakayosaidia kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza kipato cha kaya.
Naye mwakilishi wa Taasisi ya , Ndg. Perce Christian, ambaye ni Afisa Mwezeshaji katika Mradi wa Mwanamke na Ujuzi unaofadhiliwa na shirika la Swisscontact, ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa inazochukua katika kuinua uchumi wa kaya kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Ndg. Perce amesema Taasisi ya kupitia Mradi wa Mwanamke na Ujuzi itaendelea kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi wanawake na vijana ili waweze kujitegemea kiuchumi ili wamudu mahitaji ya familia na watoto. Ameongeza kuwa kwa mwaka 2026, mradi huo unatarajiwa kuwafikia jumla ya akina mama Vijana 150 katika Halmashauri za Bagamoyo, Chalinze, Wilaya ya Kibaha pamoja na Manispaa ya Kibaha.