14/08/2026
Ukusanyaji wa taka zilizotenganishwa unaendelea kuimarika Mbweni, huku wakusanya taka wakifika katika kaya mbalimbali kukusanya taka zilizotenganishwa na kuweka katika vitendo mfumo wa taka sifuri.
Wakati wa ukusanyaji, wakusanya taka wanaendelea kutoa mwongozo katika kaya kuhusu namna ya kutenganisha taka katika makundi manne yaliyopangwa. Utenganishaji huu unarahisisha kazi yao na kusaidia kuzuia aina mbalimbali za taka kuchanganyika. Pia, wanapima taka zote ili kuweza kurahisisha ufuatiliaji wa kiasi kinachokusanywa, na hivyo kupata taarifa muhimu kwa ajili ya kupanga na kusimamia mfumo wa ukusanyaji na uchakataji wa taka.
Kituo cha uchakataji taka (MRF) Mbweni kina makadirio ya uwezo wa kuhifadhi na kuchakata takribani tani 85 kwa kila mzunguko. Uwezo huu unajumuisha uchakataji wa taka ozo pamoja na uhifadhi wa taka zinazoweza kurejelezwa. Kituo hiki kimeundwa kuhudumia takribani kaya 3,000 na shughuli za biashara 400 katika Kata ya Mbweni, huku kikiwa na uwezo wa kufikia zaidi ya kaya 5,000 kitakapofanya kazi kwa uwezo wake kamili.
Kuanzia kaya, ukusanyaji hadi kituo cha uchakataji taka (MRF), mfumo huu unaunganisha wakazi na wakusanyaji taka katika kuhakikisha taka zinaendelea kutenganishwa na kusimamiwa ipasavyo.
cc: 📷:
…