19/08/2026
Tunawezaje kumsaidia mwanafunzi mwenzetu anapopewa adhabu iliyopitiliza?
Swali hili kutoka kwa mwanafunzi liliibua mjadala mzito wakati wa Mjadala wa Shule kwa Shule (Interschool Dialogue) uliofanyika katika wilaya za Babati Mji (Manyara) na Korogwe (Tanga).
Kupitia jukwaa hili, wanafunzi walipata fursa ya kukutana, kubadilishana mawazo, kujifunza kutoka kwa wenzao na kujadili kwa kina masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto.
Wanafunzi walitaja adhabu ya viboko iliyopitiliza kuwa moja ya aina za ukatili wanazokutana nazo shuleni. Akijibu hoja hiyo, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Bi. Elitruda Kashuku, aliwasisitiza wanafunzi kutumia sanduku la maoni la “Sauti Yangu” au kupiga namba 116 kutoa taarifa wanapokutana na vitendo vya ukatili dhidi yao au wenzao, ili waweze kupata msaada na hatua stahiki kuchukuliwa. Aidha, aliwakumbusha na kuwasisitiza walimu kuzingatia sheria na taratibu za utoaji wa adhabu kwa wanafunzi, ili kuhakikisha shule zinakuwa sehemu salama kwa kila mtoto kujifunza na kustawi.
Kupitia mijadala hii, tunaendelea kujenga sauti ya mtoto, kuimarisha ushiriki wa wanafunzi, na kuweka mazingira salama ya kujifunzia ambapo kila mtoto analindwa, anasikilizwa, anaheshimiwa, na anaweza kutoa taarifa bila hofu.
Mjadala huu umewezesha wanafunzi kutoka shule 10 za msingi na sekondari zinazotekeleza Mradi wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia katika Elimu (MMUKE/GET) kuwa mabalozi wa ulinzi wa mtoto
K**a mzazi/mlezi au mdau wa elimu, unaona tunapaswa kufanya nini ili kuhakikisha nidhamu shuleni inalindwa bila kuwavunjia watoto haki zao au kuwafanyia ukatili? Tushirikishe mtazamo wako kwenye maoni!