30/05/2026
Waandishi wa habari wakongwe nchini, Dkt. Maurice Samwilu Mwaffisi na Simon Martha Mkina wa gazeti la mtandaoni la Pambazuko, wameandika historia mpya baada ya kutwaa tuzo mbili za juu zaidi katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), mashindano yanayotambuliwa kuwa yenye hadhi kubwa zaidi katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Dkt. Mwaffisi, ambaye ni mwandishi, mwalimu na kiongozi mwenye uzoefu wa muda mrefu katika tasnia ya habari, alitangazwa mshindi wa Tuzo ya Mafanikio ya Maisha katika Uandishi wa Habari (Lifetime Achievement in Journalism Award - LAJA) 2025. Tuzo hiyo hutolewa kwa wanahabari waliotoa mchango mkubwa na wa kudumu katika maendeleo ya taaluma, ikiwemo kufundisha waandishi, kuandika vitabu vya taaluma ya habari, kulea waandishi wachanga, kuongoza vyumba vya habari, kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuimarisha misingi ya taaluma nchini.
Kwa upande wake, Simon Mkina alitangazwa Mwandishi Bora wa Mwaka 2025, baada ya kuwashinda Sanula Athanas wa gazeti la Nipashe na Abdallah K***a wa ITV, ambao pia walikuwa wamefika hatua ya mwisho ya kinyang’anyiro hicho.
Mkina alijizolea ushindi huo kutokana na ubora wa kazi zake za uandishi zilizokuwa na athari kubwa kwa jamii, kuzingatia viwango vya juu vya taaluma na maadili ya uandishi wa habari, pamoja na kuonyesha ubunifu na mchango wa kipekee katika mwaka 2025.
Washindi hao wawili walikabidhiwa hundi za mfano zenye thamani ya shilingi milioni tatu kila mmoja k**a sehemu ya kutambua mchango wao katika taaluma ya habari.
Kilele cha Tuzo za EJAT 2025 kilifanyika Mei 29, 2026, katika ukumbi wa Hoteli ya Four Points by Sheraton (New Africa), jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari na kurushwa mubashara kupitia Azam TV pamoja na majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.