28/03/2026
Upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa bado ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za afya ya umma na maendeleo nchini Tanzania. Katika jiji la Dar es Salaam linalokua kwa kasi, hasa katika makazi yasiyo rasmi na maeneo ya pembezoni mwa jiji, pamoja na katika jamii za vijijini kote nchini, mamilioni ya watu bado wanategemea vyanzo vya maji visivyo salama na visivyoaminika kwa mahitaji yao ya kila siku.
Ingawa visima vya maji vina mchango muhimu katika kuziba pengo la upatikanaji wa maji jijini Dar Es Salaam, ubora wa maji yanayotolewa kutoka katika vyanzo hivi mara nyingi huathiriwa na uchafuzi unaotokana na shughuli za binadamu, mazingira, pamoja na miundombinu duni ya usafi wa mazingira. Hivyo, upatikanaji wa maji pekee hauhakikishi usalama; hata vyanzo vilivyoboreshwa vinaweza kuwaweka watumiaji katika hatari kubwa za kiafya.
Kimataifa, bado mamia ya mamilioni ya watu hawapati maji ya kunywa yanayosimamiwa kwa usalama na serikali zao, hali inayowalazimu kutegemea maji ya mito, mabwawa, visima vya kienyeji, au maji yanayosambazwa kupitia mifumo isiyo rasmi.
Nchini Tanzania, hasa jijini Dar Es Salaam hali hii inaonekana zaidi miongoni mwa watu wa kipato cha chini, ambapo uhaba wa maji unahusiana moja kwa moja na umaskini, ukuaji wa haraka wa miji, na uwekezaji mdogo katika miundombinu. Madhara yake ni makubwa mno, kwani Magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama, hasa magonjwa ya kuhara, bado ni sababu kuu ya magonjwa na vifo, hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Kwa hakika, maji yasiyo salama na ukosefu wa usafi wa mazingira huchangia vifo vya watoto wengi zaidi kuliko malaria, UKIMWI, na surua kwa pamoja.
Vifo hivi vinaweza kuzuilika kwa kiasi kikubwa, jambo linaloonesha umuhimu wa haraka wa kuwekeza katika upatikanaji wa maji safi na salama na utunzwaji wa maji salama. Kuhakikisha upatikanaji wa maji salama ya kunywa si tu wajibu wa afya ya umma bali pia ni haki ya msingi ya binadamu inayohitajika kwa maisha yenye heshima, uzalishaji, na maendeleo endelevu. Ingawa juhudi za serikali na wadau wa maendeleo zimeleta mafanikio ya kuongezeka kwa upatikanaji wa maji na kuboresha utoaji wa huduma, bado kuna mapungufu makubwa, hasa katika kuhakikisha usalama na ubora wa maji wakati wa matumizi. Hii inaonesha umuhimu mkubwa wa uhitaji wa mbinu za kutibu maji katika ngazi ya kaya na uhifadhi salama wa maji (HWTS) k**a suluhisho linalokamilisha mifumo ya maji kutoka katika chanzo hadi katika matumizi ya kaya.
Miongoni mwa mbinu mbalimbali rahisi za kutibu na kuboresha maji ya kunywa katika ngazi ya familia zinazopatikana, ni Teknolojia ya kutibu Maji kwa Mionzi ya Jua (SODIS); ni njia rahisi, nafuu, na inayopatikana kwa urahisi yenye uwezo mkubwa wa kuleta matokeo kwa kutumia rasilimali chache. Njia hii inahusisha kujaza maji yenye uchafu mdogo katika chupa ya plastiki wazi (PET) na kuyaweka kwenye mwanga wa moja kwa moja wa jua kwa masaa sita au zaidi. Kupitia mchanganyiko wa mionzi ya ultraviolet (UV-A) na joto, vijidudu hatarishi, ikiwemo bakteria, virusi, na vimelea vyote, huangamizwa kabisa, na kufanya maji kuwa salama zaidi kwa matumizi. SODIS haihitaji gharama kubwa, haihusishi matumizi ya kemikali, na hutegemea vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira yote, jambo linaloifanya kuwa chaguo bora kwa jamii zilizo pembezoni.
Shirika la Wells of Life Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kuboresha hali ya maji, usafi wa mazingira, na afya (WASH) kwa kuunganisha maendeleo ya miundombinu na suluhisho za kutibu maji katika ngazi ya jamii, hasa kwenye vituo vya nyumba za watoto (Orphanage). Kazi yake inalenga si tu ujenzi na ukarabati wa vyanzo vya maji, bali pia kuhamasisha mabadiliko ya tabia yanayowawezesha kaya kudhibiti ubora wa maji wanayotumia.
Katika maeneo ambayo ujenzi wa visima hauwezekani au ambapo vyanzo vilivyopo si salama, matibabu ya maji katika ngazi ya kaya huwa ni mbadala muhimu. Pamoja na faida zake, SODIS pia ina changamoto zake. Masuala k**a kupungua kwa ufanisi kutokana na uchakavu wa chupa, ufuasi mdogo wa watumiaji, na ushindani kutoka kwa teknolojia mpya yanapaswa kuzingatiwa.
Kwa ujumla, hakuna mbinu moja ya kutibu na kuboresha maji ya kunywa katika ngazi ya familia inayofaa kila mahali; kila moja ina faida na mapungufu yake. Hivyo basi, ni muhimu kutumia mkakati jumuishi na wenye mchanganyiko wa mbinu mbalimbali unaowezesha watumiaji kufanya maamuzi sahihi kulingana na mahitaji yao.
Waraka huu umechunguza nafasi ya SODIS katika muktadha mpana wa suluhisho ya kutibu maji pembezoni mwa jiji la Dar Es Salaam na Mji mdogo wa Mikumi- Morogoro, ikilenga matumizi yake, ufanisi wake, na uwezo wake wa kupunguza mzigo wa magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama. Kwa kuzingatia vipengele vya kiufundi na kitabia vinavyohusiana na usalama wa maji, inalenga kuchangia katika mfumo imara zaidi, jumuishi, na unaolenga afya katika usimamizi wa rasilimali za maji; mfumo unaohakikisha kuwa hakuna jamii inayobaki nyuma katika jitihada za kupata maji salama ya kunywa
By Fred George